Historia
Utangulizi
Parokia ya Mt. Monika –Buhongwa ilianza kama Kigango kilianzishwa mwaka 1974 ikiwa chini ya Parokia ya Mt. Karoli Lwanga - Nyegezi. Mwaka huo 1974 ndipo aliyekua katibu kata wa kata ya Buhongwa ndugu Charles Mayunga aliposaidia kupatikana kwa maeneo mawili ya kanisa yaani eneo lilipo kanisa kwa sasa na eneo la makaburi. Wakati huo huduma ya Misa ilikua ikitolewa mara moja kwa mwezi na Padre Thomas Bulabo toka Parokia ya Bugando na ilikuwa ikiadhimishwa katika madarasa ya shule ya Msingi Buhongwa ikijumuisha waumini toka maeneo ya Lwanhima, Sahwa, Bulale, na Buhongwa yenyewe.
Ujenzi wa Kanisa
Baada ya kutumia madarasa kwa miaka kadhaa Padre Karoli toka Parokia ya Nyegezi alianzisha mkakati wa kujenga kanisa la Mt. Monika Buhongwa.
Ujenzi wa kanisa ulianza 1988 kwa kutumia tofali za tope kabla ya Padre Karoli wa parokia ya Nyegezi kuanzisha mkakati wa ujenzi wa kanisa la sasa. Katika ujenzi huo Padre Karoli alichangia fedha na vifaa vya ujenzi na waumini walichangia nguvu kazi, mawe, mchanga na ufyatuaji tofali. Ujenzi huu wa kanisa ulikamilika mwezi Agosti 1990 na uzinduzi wa Kigango ulifanywa na aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mwanza hayati Renatus Budobudo Butibubage mwezi Septemba 1990. Wakati huo kigango kilikuwa na Jumuiya 9 tu. Kigango kiliendelea kukua hali iliyopelekea waamini kununua maeneo jirani na ilipofika mwaka 2001 upanuzi wa kanisa la sasa ulianza.
Huduma za Kiroho
Kabla na baada ya uzinduzi wa kigango cha Mt. Monika mwaka 1990 huduma zote za kiroho zilikuwa na ziliendelea kutolewa na mapadre kutoka Parokia ya Bugando, Nyegezi, na Chuo cha Nyegezi Social Training Institute (NSTI) ambacho kwa sasa ndicho Chuo Kikuu cha Mt. Augustino (SAUT). Mwaka 2007 ilizinduliwa Parokia ya Mt. Agustino Mkolani na kigango cha Mt. Monika kikawa ni moja ya vigango vilivyounda Parokia hii.
Hadhi ya Parokia Teule
Mhasham Askofu Mkuu Yuda Thadeus Ruwa’ichi alikitangaza kigango cha Mt. Monika kuwa Parokia teule tarehe 27/08/2014. Wakati huo kigango kilikuwa na Jumuiya 40.
Parokia kamili
Mhasham Baba Askofu Mkuu Yuda Thadeus Ruwa’ichi wa jimbo kuu la Mwanza aliisimika rasmi Parokia ya Mt. Monika - Buhongwa siku ya Jumatano tarehe 21/12/2016.
Kiutawala
Parokia hii inaundwa na kata za Buhongwa na Lwanhima ambazo ni miongoni mwa kata zinazounda wilaya ya Nyamagana iliyopo mkoani Mwanza.
MAWANDAN YA KIUTAWALA
Parokia ya Mt. Monica iliposimikwa tarehe 21/02/2016, kulikuwa na vigango vine (4) ambavyo viliunda Parokia ya Mt. Monica. Kutokana na maendeleo katika nyanja mbalimbali na idadi ya waamini, kwa sasa kilichokuwa kigango cha Bulale, sasa ni Parokia, na kilichokuwa kigango cha Sahwa nacho kwa sasa ni Parokia. Hivyo, Kigango cha Tatu ni Kigango cha Lwanhima na amabacho kiko Parokia ya Mt. Bathoromeo Sahwa na Kigango cha nne ni Kigango cha Mt. Monica, Buhongwa na ambacho ndicho Kigango mama na muhimili mkuu wa Parokia.
Kwa sasa Parokia ya Mt. Monica Buhongwa ina jumla ya Kanda 10 na Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo 63.